Mwanamuziki wa Tanzania Seif Shaban maarufu kama Matonya, ameachiliwa kwa dhamana hii leo kufuatia kesi ya ubakaji inayomkabili humu nchini Kenya.
Mahakama iliridhia ombi la mwanamuziki huyo wa Bongo fleva la dhamana na sasa ataendelea kuwa huru huku kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Matonya amesema “Kwanza nimshukuru Mungu, leo nimepata nafasi ya dhamana na kuwa nje nikiwa katika Mahakama ya Kenya.”
Aliendelea kwa kushukuru raia wenzake wa Tanzania ambao anasema walimwombea kwa ushirikiano na ndugu zake wa Kenya. Alitaja pia familia yake ambayo anasema imepambana sana hadi walipofikia kwenye kesi hiyo bila kusahau wadau wa kikazi.
Aidha, Matonya amesema hatakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa sasa kwa kuwa liko Mahakamani ambapo ameongeza kuwa waliotekeleza jambo hilo wanajua walichokuwa wanakifanya na malengo yao.
Matonya wa umri wa miaka 43, tayari amekanusha mashtaka dhidi yake mahakamani na akakubaliwa ombi la dhamana la shilingi laki tano pesa za Kenya na inaonekana leo ndio ametimiza masharti ya dhamana na kuachiliwa.