Mwili wa marehemu Cynthia Shange, mwigizaji mkongwe wa Afrika Kusini, ulizikwa wikendi iliyopita katika hafla ya faragha katika eneo la vilima la Inanda, KwaZulu-Natal.
Shange alifariki Aprili 20, 2026 akiwa na umri wa miaka 76, baada ya kuugua kwa muda mfupi huku kifo chake kikihisiwa katika tasnia ya uigizaji nchini Afrika Kusini.
Binti ya marehemu Cynthia Shange aitwaye Nonhle Thema ambaye ni mwanahabari ndiye alitangaza kifo cha mama huyo kupitia akaunti yake ya Instagram. Aliandika, “Pumzika Malkia. Asante kwa kuwa mama yetu”.
Familia ya mwendazake iliamua kwamba hata ingawa alikuwa maarufu, mazishi yake yangekuwa ya faragha, mbali na kelele za mitandao ya kijamii ambapo walisherehekea maisha yake alikozaliwa.
Thema baadaye alimwelezea marehemu mamake kama “moyo wenye neema na huruma.”
Mwaka 1972, katika kilele cha ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Mama Shange alikua mwanamke wa kwanza mweusi kuwahi kuwakilisha Afrika Kusini katika jukwaa la kimataifa aliposhiriki mashindano ya urembo ya Miss World 1972 jijini London chini ya taji la Miss Africa South.
Wakati huo mashindano hayo hayakuhusu tu urembo, yalihusu ujasiri wa kupinga, utambulisho na kuonekana katika enzi iliyokusudia kufuta ubora wa watu weusi.
Ushindi wake kama mshindi wa kwanza mweusi wa taji la Miss South Africa ulibadili kabisa taswira ya urembo katika taifa lililogawanyika.
Leo, uwakilishi mara nyingi hujadiliwa katika mikutano ya mauzaji na mijadala ya jukwaani, lakini Mam’Shange aliishi hilo wakati hatari zilikuwa kubwa zaidi.