Mwanamuziki wa Uganda Spice Diana amejipata akizungumziwa sana kufuatia hatua yake ya kutwaa vifaa vya eneo moja la burudani katika wilaya ya Bukomansimbi katikati mwa Uganda, kwa kukosa kulipwa.
Inaripotiwa kwamba mrembo huyo aliondoka na vipakatalishi, vipaaza sauti, spika na vifaa vingine baada ya aliyemwalika kutumbuiza katika eneo husika kukosa kukamilisha malipo yake.
Video iliyosambaa mitandaoni, inamwonyesha Diana akisimamisha tumbuizo jukwaani na kuonya hadharani kwamba iwapo hangelipwa angekomesha tumbuizo na kuondoka na vifaa.
Akijitetea jukwaani, Spice Diana ambaye jina lake halisi ni Namukwaya Hajara Diana, alisema kwamba yeye ni mpenda amani na mtulivu kutegemea na vile anavyochukuliwa.
“Nitachukua vifaa ambavyo thamani yake ni sawa na pesa ninazodai. Leo mtaniua kutoka hapa,” alisema mwanamuziki huyo ambaye alikubali kukamilisha tumbuizo lakini akakataa kuondoka bila malipo.
Alisema kwamba ana wafanyakazi wa kulipa na kwamba muziki ndio njia yake ya pekee ya kujipatia kipato na usimamizi wa eneo hilo la burudani ulikusanya ada ya kiingilio kutoka kwa wahudhuriaji.
Alipomaliza kutumbuiza alionekana akibeba vifaa kabla ya kuondoka jukwaani.
Baadaye kwenye mtandao wa kijamii wa Snapchat aliandika, “Watu wa kawaida wanafurahia vitanda vyao unaendesha gari masaa manne, unateseka na barabara mbaya za Uganda usiku wa manane alafu ati hakuna malipo”.