Azziad Nasenya apatiwa ubalozi wa Maybelline New York

Alitambulishwa rasmi Aprili 25, 2026 katika hafla ya faragha iliyohudhuriwa na watu kadhaa maarufu.

Marion Bosire
2 Min Read

Azziad Nasenya ameandikisha historia baada ya kuteuliwa kuwa msemaji wa kidijitali au ukipenda balozi wa kampuni ya vipodozi ya Maybelline New York katika eneo la kusini mwa Sahara barani Afrika.

Mrembo huyo ambaye umaarufu wake ulitokana na mtandao wa TikTok, sasa anakuwa raia wa kwanza wa eneo la Afrika Mashariki kuwahi kuhudumu katika nafasi kama hiyo na kampuni ya ulimwengu mzima ya urembo.

Nasenya ambaye pia ni mwigizaji alitaja hatua hiyo kuwa zaidi ya jina akiitaja kuwa mabadiliko makubwa katika uwakilishi huku urembo wa Afrika, masimulizi na sauti vikipata utambuzi katika jukwaa la ulimwengu.

Katika kampuni hiyo ya Maybelline New York, msemaji wa kidijitali anahudumu kama balozi katika eneo fulani ambaye anaangazia maudhui halisia na mikakati ya mauzaji kidijitali.

Tofauti na mabalozi wa dunia au wasemaji wa dunia ambao wanaweza kuongoza kampeni za televisheni na gazeti, msemaji wa kidijitali huchaguliwa au kuteuliwa kuwakilisha nembo husika katika mitandao ya kijamii kama TikTok, Instagram na YouTube, lengo likiwa kutagusana kwa undani na hadhira ya kisasa.

Nasenya alitambulishwa rasmi Aprili 25, 2026 katika hafla ya faragha iliyohudhuriwa na watu kadhaa maarufu ambao walikuwa wamevaa mavazi ya rangi ya njano na pinki rangi rasmi za Maybelline New York.

Haya yanajiri miezi kadhaa baada ya taarifa kuibuka kwamba ufukara ulikuwa umemsibu mrembo huyo na kwamba nyumba yake ingepigwa mnada.

Share This Article