Upendo Nkone atoa wimbo mpya baada ya kuzawadiwa gari

Mashabiki walichanga wakamnunulia gari baada ya ugomvi na Martha Mwaipaja

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili wa Tanzania Upendo Nkone ametoa wimbo mpya, siku chache tu baada yake kutunukiwa zawadi ya gari na mashabiki wake.

Wimbo huo unaitwa “Narudidha Sifa” na kulingana na Upendo, aliona kwamba hawezi kunyamaza hasa baada ya kushuhudia udhihirisho wa upendo wa Yesu kwa namna ya kipekee kupitia zawadi hiyo.

Wimbo huo unalenga kukumbusha watu kwamba kila baraka sio kwa uwezo wao, bali ni neema ya Mungu na hivyo wanapaswa kurudisha sifa zote kwake.

Iwapo ulikosa yaliyojiri, kulikuwa na zogo kati ya Upendo Nkone na mwimbaji mwenza Martha Mwaipaja ambaye huwa anmrejelea kama binti yake kiroho.

Upendo alisikika kwenye mahojiano akisema kwamba Martha alimpigia simu na kumtishia baada yake kujaribu kusema naye kufuatia mzozo uliozuka kati ya Mwaipaja na familia yake.

Nkone anasema aliombwa na mama mzazi wa Martha Mwaipaja aseme naye ili kusuluhisha zogo lililopo ambapo mamake Martha anadai kwamba mwanawe huwa hamshughulikii inavyostahili.

Martha alikanusha madai ya kumpigia Nkone simu na kumtishia huku Joan ambaye Martha anamrejelea kama mwanawe akiingilia kati na kumtusi Nkone akisema kwamba yeye ni fukara hana chochote hata bajaji ya usafiri.

Kauli hizo za Joan mwanawe Martha Mwaipaja zilichochea mashabiki kuchanga pesa na kumnunulia Upendo Nkone gari wakiongozwa na Resty Bura na Lilian Mwasha.

Waliandaa hafla kubwa ya kumkabidhi gari hilo Alhamisi Aprili 23, 2026 katika ukumbi wa Mlimani City, hafla ambayo kwa wakati mmoja ilibadilika na kuwa mkutano wa kumsifu na kumwabudu Mungu.

Upendo Nkone na Martha Mwaipaja walipatanishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila hata kabla ya siku ya kumkabidhi gari. Mwaipaja alialikwa kwa hafla hiyo lakini hakuhudhuria.

Share This Article