Wapinzani wawili wakubwa wa kisiasa wa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu wameungana katika jitihada za kuiondoa serikali yake ya muungano katika uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Mawaziri wakuu wa zamani Naftali Bennett wa mrengo wa kulia na Yair Lapid wa mrengo wa kati walitoa taarifa Jumapili wakitangaza muungano wa vyama vyao.
Wanalenga kuunganisha upinzani uliogawanyika ambao unaonekana kuwa na mambo machache yanayofanana zaidi ya uhasama wao wa pamoja dhidi ya Netanyahu.
Afisi ya Bennett ilisema chama kipya kitaitwa “Together” na kwamba yeye ndiye atakayekuwa kiongozi wake.
“Ninafuraha kutangaza kwamba usiku wa leo, pamoja na rafiki yangu Yair Lapid, ninachukua hatua ya kizalendo na ya Kizayuni zaidi ambayo tumewahi kuchukua kwa ajili ya nchi yetu,” Bennett alisema katika taarifa ya pamoja na Lapid iliyorushwa moja kwa moja.
Wakati wa taarifa hiyo ya televisheni, Lapid alisema, “Bennett ni mwanasiasa wa mrengo wa kulia, lakini ni mwaminifu na kuna uaminifu kati yetu.”
Bennett alisema akichaguliwa, ataunda tume ya kitaifa ya uchunguzi kuhusu kile anachokiita kushindwa kulikosababisha shambulio la tarehe 7 Oktoba 2023 lililoongozwa na Hamas, jambo ambalo serikali ya sasa ya Netanyahu imekataa.
Lapid na Bennett wamekuwa wakosoaji wakubwa wa namna Netanyahu alishughulikia vita vya nchi tangu shambulio hilo, huku Lapid akielezea usitishaji vita wa wiki mbili uliokubaliwa na Iran kama “janga la kisiasa”.
Bennett na Lapid wamewahi kuungana awali, wakimaliza utawala wa miaka 12 mfululizo wa Netanyahu katika uchaguzi wa 2021, lakini wakaunda serikali ya muungano iliyodumu kwa takribani miezi 18 tu.
Kabla ya hapo, waliingia kwa nguvu katika serikali ya muungano ya mwaka 2013 katika hatua iliyowaacha nje washirika wa jadi wa Netanyahu wa Kiyahudi wenye msimamo mkali wa kidini.
Netanyahu, ambaye ndiye Waziri Mkuu wa Israeli aliyedumu kwa muda mrefu zaidi madarakani, alirejea madarakani aliposhinda uchaguzi wa Novemba 2022 na kuunda serikali yenye mrengo wa kulia zaidi katika historia ya Israeli.