Tanzania kuandaa Miss World 2027

Makubaliano kuhusu hatua hii yalitiwa saini siku moja tu baada ya Tanzania kumvisha taji Miss World Tanzania.

Marion Bosire
2 Min Read
Latricia Ian, Miss World Tanzania 2026

Tanzania ndiyo itakuwa mwenyeji wa mashindano ya ulimwengu ya ulimbwende almaarufu Miss World 2027.

Haya yaliafikiwa siku moja tu baada ya Tanzania kumvisha taji mlimbwende Latricia Ian wa umri wa miaka 24, ambapo Tanzania ilitia saini mkataba wa maandalizi na kuwa nchi ya pili barani Afrika kuandaa mashindano hayo baada ya Afrika Kusini.

Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Paul Makonda alishuhudia kutiwa saini kwa makubaliano hayo ya kuandaa mashindano ya Miss World mwaka 2027 akitaja tukio hilo kama jukwaa la kuonyesha mazuri ya Tanzania.

Alitaja utalii, fursa za uwekezaji, utamaduni na talanta kuwa baadhi ya vitu ambavyo Tanzania itaonyesha ulimwengu kupitia mashindano hayo mwakani.

Nchi zipatazo 130 zinatarajiwa kushiriki mashindano hayo ya urembo huku matukio yake yakitarajiwa kufikia watazamaji zaidi ya bilioni 2 wa runinga kote ulimwenguni.

Waandalizi wa mashindano hayo wamebashiri kwamba wageni wapatao elfu 20 wa kimataifa watahudhuria tukio hilo ambalo litadumu mwezi mzima.

Litajumuisha hafla ya makaribisho, maonyesho ya talanta, shughuli za kusaidia jamii, maonyesho ya mitindo ya mavazi pamoja na hafla ya fainali.

Mwenyekiti na Afisa Mkuu Mtendaji wa Miss World Limited Julia Morley alisema mashindano hayo yana uwezo wa kuendesha utalii, kutoa fursa za ajira na kuinua hadhi ya Tanzania kama eneo la utalii na uwekezaji.

Share This Article