Miamba wa soka nchini Kenya Gor Mahia wangali wanashikilia kukutu uongozi jedwali la Ligi kuu ya Kenya zikisalia mechi sita msimu ukamilike.
Licha ya kutoka sare tasa katika mechi ya Jumapili dhidi ya Bandari,Gor wanaongoza msimamo kwa alama 58, kutokana na michuano 28 ,pointi 3 nyuma ya AFC Leopards wanaokalia nafasi ya pili.
Mabingwa watetezi Police FC wanakalia nafasi ya tatu kwa pointi 47 ,alama moja zaidi ya Kakamega Homeboyz na Shabana FC zilizo katika nafasi za nne na tano mtawalia.
Kinyang’anyiro cha kusalia ligini kinazidi kuwa kigumu huku timu za APS Bomet,Ulinzi Stars,Kariobangi Sharks,Bidco United na Sofapaka zikijizatiti kujisalimisha.
Sofapaka inaburura mkia kwa pointi 17 alama 5 nyuma ya Bidco wakati Sharks ikiwa ya tatu kutoka mkiani kwa pointi 26.