Dufla Diligon, msanii wa muziki wa mtindo wa dancehall and Afro-pop amemjibu mwanamuziki mwenza Nadia Mukami kuhusiana na ombi la mrembo huyo la kufutwa kwa wimbo “Side Chick”.
Diligon ambaye jina lake halisi ni David Long’oji Ekiru alishirikiana na Arrow Bwoy au ukipenda Ali Yusuf ambaye ni mume wa Nadia katika kuandaa wimbo huo wa kusifia Side Chick.
Wimbo huo haukumfurahisha Nadia ambaye anahisi hauna heshima, akitaka ufutwe.
Sasa Dufla anasema kwamba hataridhia ombi hilo hadi pale ambapo Nadia Mukami atamlipa shilingi milioni 2, gharama ya maandalizi ya wimbo huo.
Kando na jibu hilo, Diligon alimtaka Nadia awasilishe malalamishi yake kwa mume wake Arrow Bwoy moja kwa moja.
Awali Arrow Bwoy alikuwa amejibu ombi la Nadia bila hata kumtaja akielekeza mgogoro huo kwa mashabiki zake ambapo aliwaomba ushauri kuhusiana na wimbo huo wa “Sidechick”.
Alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii akitaka kufahamu iwapo ukweli wimbo huo unakosea watu fulani heshima.
“Hamjambo natumai nyote mko salama, mimi ni Arrow Bwoy, niko hapa kwanza kuwashukuru kwa kuunga mkono kazi yetu ya hivi karibuni zaidi…” Alisema Arrow Bwoy kwenye video hiyo.