Waziri wa Fedha wa Tanzania, Khamis Mussa Omar, amefanya mazungumzo ya kina na Mkuu wa Ofisi ya Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Nick Checker.
Mazungumzo hayo yaliofanyika ndani ya kuta za Ubalozi wa Tanzania jijini Washington DC, yilifanyika yakiwa ni sehemu ya mfululizo wa mikutano inayokwenda sambamba na Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (2026 IMF/WBG Spring Meetings).
Viongozi hao wawili wamejikita katika kutathmini na kuibua fursa mpya za ushirikiano wa kibiashara, huku mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye sekta ya madini ambayo ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa sasa.
Umuhimu wa mkutano huu umesisitizwa na uwepo wa maafisa waandamizi kutoka pande zote mbili. Kwa upande wa Tanzania, Waziri Omar aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Natu El-maamry Mwamba, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Aboud Hassan Mwinyi. Aidha, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Elsie Sia Kanza, alishiriki kikamilifu katika kuratibu na kufanikisha mazungumzo hayo.