Gavana Lusaka avunja Baraza la Mawaziri

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Bungoma Ken Lusaka, avunja Baraza la Mawaziri.

Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka, amevunja Baraza la Mawaziri pamoja na kuwafurusha Mwanasheria Mkuu na Katibu wa Kaunti, katika kile alichokitaja kuwa hatua ya kufanya mabadiliko katika uongozi wa kaunti hiyo.

Kupitia kwa taarifa, Lusaka alisema hatua hiyo ilitekelezwa kuambatana na katiba, kuhakikisha utoaji huduma kwa umma unaimarishwa katika kaunti ya Bungoma.

“Kuambatana na sehemu ya 40(1)(a) ya serikali za kaunti, mawaziri wote wa kaunti, Mwansheria Mkuu na Katibu wa kaunti wameondolewa afisini mara moja,” ilisema taarifa hiyo.

Kulingana na Lusaka, hatua hiyo ilitekelezwa kwa maslahi ya umma, akidokeza kuwa mabadiliko hayo yanalenga kulainisha operesheni katika usimamizi wa kaunti hiyo na kulinda uadilifu wa kitaasisi.

Lusaka alisema mawasiliano kuhusu watakaokaimu na uteuzi wa nyadhifa hizo yatatangazwa kwa kuzingatia sheria.

Aidha, aliwashukuru maafisa hao wanaoondoka kwa huduma walizotoa, alikariri kujitolea kwa utawala wake kuzingatia katiba na mfumo sheria.

Share This Article