Polisi walaumiwa kwa kufanikisha biashara ya mihadarati

Haya yaliibuka katika kikao cha kamati ya bunge la taifa kuhusu utawala na usalama

Marion Bosire
3 Min Read
Dido Raso, Mwenyekiti, Kamati ya Bunge Kuhusu Utawala na Usalama

Kamati ya bunge la taifa kuhusu utawala na usalama, imelaumu polisi kwa kile ilichokitaja kuwa kufanikisha biashara ya pombe haramu na mihadarati nchini.

Haya yaliibuka katika kikao cha kamati hiyo na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, Mohammed Amin na yule wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya, NACADA, Anthony Omerikwa.

Mbunge wa Homa Bay mjini Peter Kaluma alisema kwamba anafahamu wanafunzi wa vyuo vikuu huko Nyanza wanapata dawa fulani kutoka Ethiopia ambayo huagizwa na kusafirishwa chini ya uangalizi wa polisi.

Mwenzake wa Kisumu Magharibi Rosa Buyu naye alitoa maoni sawia akisema kwamba pombe haramu huingizwa nchini kutoka Uganda na inalindwa na polisi na kwamba polisi huuza pombe haramu inayokamatwa.

DCI hata hivyo ilisisitiza kwamba huduma ya taifa ya polisi haikubalii kamwe ulanguzi wa dawa za kulevya na kwamba maafisa wachache wapotovu huchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Huduma ya taifa ya polisi haikubalii ulanguzi wa pombe na mihadarati. Huduma hii imefanya vyema katika vita dhidi ya uovu huo,” Amin alitetea polisi akisema hata polisi wenyewe ni waathiriwa wa uraibu wa pombe na mihadarati.

Katika kikao cha leo, Amin na Omerikwa walitakiwa kuelezea mikakati waliyoweka ili kuimarisha vita dhidi ya mihadarati tangu wakati Rais William Ruto alitangaza tatizo hilo kuwa dharura ya kitaifa.

Mkurugenzi wa DCI alisema kwamba huwa wanatekeleza misako ya kila mara akipendekeza haja iliyopo ya kuimarisha uwezo wa kitengo cha polisi cha kukabiliana na mihadarati.

Kulingana naye, walanguzi wa dawa za kulevya sasa wanatumia majukwaa ya dijitali kuendeleza biashara zao hali inayofanya iwe vigumu kupambana na uovu huo.

Omerikwa naye alisema kwamba NACADA inaunga mkono pendekezo la sheria ambayo itaongeza umri halali wa kutumia pombe kutoka miaka 18 hadi miaka 21 kwani vijana ndio waathiriwa wakuu wa uraibu wa dawa za kulevya.

Aliongeza kwamba wameimarisha ufuatiliaji katika taasisi za elimu ya juu ambazo zimegeuka kuwa vituo vya biashara ya mihadarati akipendekeza uwekezaji zaidi ili kubuni vituo zaidi vya matibabu na urekebishaji tabia kwa waraibu wa mihadarati kote nchini.

“Kuna vituo 6 pekee vya umma vya urekebishaji tabia nchini, vingine 129 ni vya kibinafsi. Kaunti 9 hazina kabisa vituo vya kurekebisha tabia,” alisema Omerikwa akihimiza uwekezaji zaidi.

Wanachama wa kamati hiyo ya utawala na usalama walizua maswali kuhusu jinsi DCI na NACADA zinashughulikia uagizaji wa bangi kutoka mataifa jirani ambayo yamehalalisha matumizi yake.

Amin alisema kwamba wanashirikiana na serikali za nchi jirani na wamepiga hatua kubwa katika kukabiliana na ulanguzi wake na wanatekeleza oparesheni za kila siku kukabiliana na tatizo la mihadarati.

Disemba 31, 2025 katika hotuba yake ya kukaribisha mwaka mpya wa 2026, Rais William Ruto alitangaza matumizi ya pombe na mihadarati kuwa dharura ya kitaifa ambapo aliangazia pia mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na tatizo hilo.

Share This Article