Tamasha la mwaka huu la Wireless nchini Uingereza limefutiiwa mbali, baada ya aliyekuwa amepangiwa kuwa msanii mkuu Kanye West kuzuiwa kuingia nchini humo.
Waandalizi wa tamasha hilo walitoa taarifa fupi kwenye akaunti iliyothibitishwa ya Wirelessfest kwenye Instagram wakisema, “Kutokana na hatua ya serikali ya kumfungia kabisa Kanye kuingia Uingereza, tumelazimika kusitisha tamasha la Wireless.”
Taarifa hiyo ilisema pia kwamba wote ambao walikuwa wamelipia tamasha hilo watarejeshewa pesa zao zote, wakiongeza kwamba wadau kadhaa walikuwa wameshauriwa kabla ya kuafikia Kanye kuwa msanii mkuu wa awamu ya mwaka huu ya tamasha la Wireless.
Wadau hao kwa wakati huo hawakuwa na pingamizi kumhusu msanii huyo wa Marekani ambaye kwa miaka mingi amezua ghadhabu kwa kutoa matamshi ya chuki dhidi ya Wayahudi.
Waandalizi hao wanakiri kwamba matamshi ya chuki huchukiza na wametambua athari za matendo ya msanii huyo mkubwa huku Kanye mwenyewe akisema kwamba anatambua maneno tu hayatoshi na anatumai kupata fursa ya kuanzisha mazungumzo na jamii ya Wayahudi nchini Uingereza.
Uuzaji wa tiketi za mapema za tamasha hilo ulianza Jumanne saa sita mchana na inaaminika kwamba ziliisha zote na mauzo ya tiketi zote yalitarajiwa kufanyika Jumatano.
Wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza ilithibitisha kwamba Kanye alituma maombi Jumatatu ya kusafiri hadi Uingereza kupitia mfumo wa kuidhinisha usafiri kielektroniki.
Ilisema uamuzi wa kumnyima fursa ya kuingia Uingereza unatokana na imani kwamba uwepo wake nchini humo haungekuwa bora kwa umma.
Kampuni zilizokuwa zikidhamini tamasha hilo za Pepsi na Diageo zilijiondoa kwenye tamasha la mwaka huu la Wireless baada ya Waziri Mkuu Kier Starmer kupinga ujio wa Kanye.