Dudu Baya aghadhabishwa na wasanii wa kiume kuvaa kike

Anahimiza vijana wasiigize wasanii wenye tabia kama hiyo.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muda mrefu wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania Godfrey Tumaini au Dudu Baya anaonekana kughadhabishwa na mtindo ambao unaendelea kukubalika wa wasanii wa kiume kuvaa mavazi ya kike.

Dudu Baya ambaye mara nyingi hukosoa maovu katika jamii alionyesha kutoridhika kwake kupitia video aliyochapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Alianza kwa kuelezea jinsi mwaka 2017, alimkemea mwanamuziki mwenza Diamond Platnumz kwa kuvaa vikuku kwenye miguu yote miwili, hatua ambayo kulingana naye inaashiria kwamba mtu ni shoga.

Ushauri huo anasema aliutoa kwenye mahojiano katika kipindi cha Refresh cha Wasafi Media inayomilikiwa na Diamond mwenyewe na uzuri Diamond alisikia ushauri wake na akaacha hizo tabia.

“Nilimwonya nikamwambia dogo usilete umagharibi, hii ni Tanzania kuvaa vikuku mtoto wa kiume miguu yote miwili,” alisema Dudu Baya akilalamika kwamba Diamond amelifanya tena, kwa kuvaa wigi kwenye video ya wimbo wake, “Happy”.

Dudu Baya anadai kwamba watu maarufu wanatumiwa kueneza mtindo wa maisha wa mapenzi ya jinsia moja na vijana wanaokua nchini Tanzania wanakurupuka kuiga.

Kulingana naye, Waziri Dorothy Gwajima anajiandaa kutoa tamko kali kuhusu wanaume wanaovaa mavazi ya kike akimkumbusha aangazie wasanii ambao anasema ndio chanzo cha hulka hiyo.

Alitoa mfano wa watu fulani maarufu kuvaa mavazi ya kike kwenye harusi ya mwanamuziki Juma Jux akisisitiza kwamba ukosoaji ni lazima uwepo ili kuikomboa Tanzania kutokana na kile alichokitaja kuwa Sodoma na Gomora.

“Kataeni kuiga mambo ya kijinga kwa hawa watu wanaojifanya wao ni ma star. Mheshimiwa Waziri lisimamie hili,” alisema Dudu.

Share This Article