Azawi akanusha madai ya ugomvi kati yake na Joshua Baraka

Anadaiwa kuashiria kwamba yeye ni msanii mkubwa kuliko Baraka nje ya Uganda.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa kike wa Uganda Priscilla Zawedde maarufu kama Azawi amekanusha madai kwamba kuna ugomvi kati yake na mwimbaji wa nyimbo za injili Joshua Baraka, ambaye pia ni wa asili ya Uganda.

Alikuwa akizumgumza na wanahabari ambapo alisema kwamba aliwekwa kwenye mtego na chombo fulani cha habari nchini humo na mtego huo ukamnasa kulingana na mtindo wake wa maisha.

Kulingana naye, mtego huo ulimdhihirisha kama mtu tofauti kabisa na alivyo lakini anasema haikuwa nia yake.

“Gumzo lilianzia mahali fulani ili kufikia katika kauli hiyo, lakini walikata kipande cha video na kukiwekea maelezo ambayo yalilifanya kuwa baya,” alisema Azawi.

Huku akisisitiza kwamba mashabiki wanaomfahamu wanaua kwamba tetesi hizo sio za kweli, Azawi alisema kwamba amemfahamu Joshua Baraka kwa muda mrefu hata kabla yake kuwa nyota na ni kama kakake.

“Yeye ni shabiki wangu nami ni shabiki wake mkubwa. Sote tunafanya vyema katika njia zetu tofauti,” alisisitiza Azawi akiongeza kwamba anajivunia Joshua Baraka.

Binti huyo alilalamika kwamba vyombo vya habari vinapenda sana kuzua mabishano kwani ndiyo njia vinajiendeleza.

Azawi aliamua kujitetea baada ya sehemu ndogo ya mahojiano yake kusambazwa mitandaoni ambapo anasikika akisema kwamba yeye ni msanii mkubwa kuliko Baraka nje ya Uganda kwa sababu mashabiki wake sio wakazi wa mijini tu kama wale wa Baraka.

Baraka alijibu madai hayo kwa ghadhabu akikosoa uchambuzi wa masuala ya sanaa akiwataka wasanii wenzake kuangazia kuunda muziki na kuachia mashabiki kazi ya kuwapima.

Share This Article