Waziri wa Nishati na Petroli Opiyo Wandayi, ameagiza kampuni ya One Petroleum Limited kuondoa shehena ya mafuta ya Petroli iliyoingiza hapa nchini kwa njia haramu.
Kupitia kwa taarifa, Wandayi pia aliagiza kampuni hiyo pamoja na kampuni zingine zilizonunua mafuta hayo, kuondoa malipo yoyote yanayotokana na mafuta hayo.
“Kampuni za uuzaji mafuta hazipaswi kulipa mafuta hayo kutoka kwa shehena hiyo,” alisema Wandayi.
Kutokana na hayo, wizara hiyo imeikataza Halmashauri ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA) dhidi ya kufanyia mabadiliko bei ya bidhaa za Petroli.
Hayo yameafikiwa huku uchunguzi ukiendelea kuhusu kuingizwa hapa nchini kwa mafuta ya ubora wa viwango vya chini, hatua iliyosababisha kujiuzulu kwa Katibu wa idara ya Nishati Mohamed Liban, Mkurugenzi Mkuu wa EPRA Kiptoo na Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Pipeline Joe Sang.
Wandayi alisema metric tani 60,000 ya mafuta ya super petrol pia yalihatarisha uadilifu wa mfumo uliohakikisha usalama wa usambazaji na bei dhabiti.