Timu za AFC Leopards,Nairobi United na KCB zimesajili ushindi katika mechi tatu za Ligi kuu ya Sportpesa zilizochezwa Jumapili katika nyuga tofauti.
Leopards maarufu kama Ingwe wamesajili ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Muaranga Seal na kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi ,katika mechi iliyosakatwa katika uchanjaa wa Nyayo.
Ronald Shichenje alipachika goli la kwanza dakika ya 53, kabla ya kiungo Hassan Beja, kukamilisha shughuli pevu kwa bao la dakika ya 83.
Wahifadhi hela KCB walipata ushindi wa goli moja kwa nunge ugenini kwa Bidco United katika uwanja wa Wang’uru ,goli pekee likipachikwa na Kevin Etemesi kunako dakika ya 29.
Katika uwanja wa Kasarani ,Nairobi United wameikomoa Shabana FC 3-0,Duncan Odhiambo na Michael Karamor, wakifunga magoli yote kunako kipindi cha kwanza kabla ya Mustapha Kizza kuongeza la tatu dakika za mwisho.