Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Rwanda, Olivier Kavutse, amezindua eneo jipya la burudani lenye mwelekeo wa Kikristo huko Kigali.
Lengo kuu ni kutoa mazingira tulivu kwa ajili ya mwingiliano wa kijamii, ubunifu na mapumziko.
Kituo hicho kinachojulikana kama ORA Center katika eneo la Kicukiro, jijini Kigali, kimeundwa kwa matumizi mbalimbali na kitakuwa kikiandaa shughuli za mchana na jioni, hasa kwa wabunifu na pombe haiuzwi huko.
Kavutse ambaye amekuwa mbali na ulingo wa muziki wa injili kwa kiwango kikubwa tangu alipohamia Kanada mwaka 2020, alishirikiana na kundi la Beauty for Ashes katika kubuni kituo hicho .
Alisema lengo la kuanzisha eneo hilo ni kuunda mazingira ambapo watu, hasa Wakristo, wanaweza kuungana na kufurahia maisha katika mazingira yanayoongozwa na maadili.
“Wakristo hawafurahii kabisa, nilitaka sehemu ambapo wanaweza kujiburudisha, kucheza michezo na kula chakula kizuri bila kuwa katika mazingira yaliyojaa vishawishi.” alisema Kavutse.
Msanii huyo alibainisha kuwa kituo hicho kinatoa chaguo mbadala wa maeneo ya kawaida ya burudani, kwa msisitizo mkubwa wa kudumisha maadili yanayolingana na maono yake.
Mchana watu wanaweza kutumia ORA Center kama eneo la kufanya kazi kwa pamoja, likitoa huduma ya intaneti, sehemu za kufanyia kazi, na chumba cha mazoezi kwa wabunifu.
Eneo hilo pia lina duka la kahawa, mgahawa mdogo na huduma za ushauri nasaha kwa wageni wanaohitaji mwongozo na msaada.
Jioni eneo hilo hubadilika na kuwa kitovu cha burudani, kikijumuisha michezo ya ndani kama vile pool na tenisi ya mezani, pamoja na maeneo ya shughuli za makundi na mikusanyiko ya kijamii.
Kavutse aliongeza kuwa eneo hilo lina uwezo wa kuandaa matukio mbalimbali, kama sherehe za binafsi, warsha na maonyesho madogo.
Ingawa limejikita katika maadili ya Kikristo, eneo hilo liko wazi kwa wasanii na watu binafsi wanaokuza ujumbe chanya na wenye uwajibikaji wa kijamii.