Mataifa kadhaa ya Afrika yameanzisha hatua za dharura ili kulinda chumi zao dhidi ya athari ya ukosefu wa mafuta ambayo huenda ikatokana na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati ambapo nchi nyini hununua mafuta.
Mgogoro huo unatishia kusababissha ukosefu wa mafuta kufuatia kuvurugika kwa usambazaji wa mafuta duniani kutokana na mgogoro ulioanza mwisho wa Februari mwaka huu wa 2026 baada ya Israel kwa ushirikiano na Marekani kushambulia Iran.
Meli nyingi za kusafirisha mafuta hupitia eneo dogo lililopatiwa jina la “Straight of Hormuz” ambalo sasa Iran inathibiti kwa makini zaidi kama mbinu ya kujiinda katika mzozo unaoendelea.
Mlango huo wa Hormuz ni njia muhimu kwa biashara ya nishati duniani na kufungwa kwake kumesababisha kupanda kwa kasi kwa bei ya mafuta na kufichua udhaifu wa nchi zinazotegemea uagizaji wa mafuta.
Nchini Afrika Kusini, mamlaka zilianzisha mpango wa kupunguza kwa muda matozo ya mafuta na kuimarisha usimamizi wa bei za vituo vya mafuta.
Ethiopia iliweka kipaumbele katika usambazaji wa mafuta kwa sekta muhimu huku ikitekeleza hatua za kuhifadhi nishati kama kufanya kazi nyumbani na kupunguza matumizi ya magari.
Zambia ilitangaza hali ya dharura ya kitaifa, ikasitisha ushuru wa bidhaa na kuonya kampuni za mafuta dhidi ya kuficha bidhaa, huku Zimbabwe ikiongeza mchanganyiko wa ethanol kwenye petroli ili kuongeza akiba iliyopo.
Nchini Tanzania, ufuatiliaji mkali wa maghala ya mafuta na uagizaji wa ziada umeimarishwa ili kudhibiti upatikanaji.
Katika visiwa ya Mauritius shehena za dharura za mafuta zilifikishwa huko na inaendelea kutafuta mikataba mipya ya usambazaji, huku Kenya ikidumisha bei thabiti kupitia ruzuku na kutafuta wasambazaji mbadala, ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote nchini Nigeria.
Wakati huo huo, Nigeria inaongeza uwezo wa kusafisha mafuta ili kukidhi mahitaji ya ndani na ya kikanda, ikidhihirisha nafasi yake kama mdhibiti muhimu wa soko.
Msumbiji umetumia hazina ya uthabiti kupunguza athari za kupanda kwa bei kwa watumiaji.
Barani kote, serikali zinachanganya ruzuku, punguzo la kodi, upangaji wa matumizi, na utofautishaji wa vyanzo vya usambazaji katika juhudi za pamoja kupunguza athari za kiuchumi za mgogoro huu.