Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu wa Mipaka (IEBC), imesema wapiga kura wapya 344,316 wamesajiliwa kufikia Alhamisi Aprili 2,2026.
Kupitia kwa taarifa siku ya Ijumaa, mwenyekiti wa tume hiyo Erastus Ethekon, alisema wakenya 18,610 wamebadilisha vituo vyao vya kupigia kura huku wengine 329 wakibadilisha maelezo yao.
“Tume hii inalenga kuwasajili wapiga kura wapya milioni 2.5 katika zoezi linaloendelea la usajili endelevu wa wapiga kura,” alisema mwenyekiti huyo.
Huku akisema kuwa zoezi la usajili wa wapiga kura litatekelezwa hadi wakati huu wa Siku Kuu ya Pasaka na mwishoni mwa wiki, Ethekon aliwahimiza Wakenya kujitokeza kwa wingi kujisajili, akihakikisha kuwa shughuli hii haitaongezewa muda baada ya Aprili 28, 2026.
“Baada ya zoezi hili kukamilika, usajili wa wapiga kura utatekelezwa katika afisi za maeneo bunge. Kwa hivyo wakati ni sasa wa kujisajili,” alidokeza Ethekon.
Shughuli ya usajili wa wapiga kura katika afisi za maeneo bunge ilianza Septemba 29, 2025, huku usajili endelevu wa wapiga kura ukizinduliwa Machi 30, 2026.