Diamond ajibu shutuma za kuiga kazi za wengine

Sehemu za wimbo wake wa Happy zinadaiwa kuigwa kutoka kwa nyimbo za wanamuziki wengine.

Marion Bosire
2 Min Read

Nyota wa Bongo Fleva nchini Tanzania Diamond Platnumz amezungumza kuhusu tetesi kwamba aliigiza kazi za wanamuziki wengine katika kuunda kazi yake ya hivi punde zaidi ya “Happy”.

Alikuwa akihojiwa kwenye kipindi cha Exclusive cha Wasafi Fm naye Lil Ommy ambaye alifungua mahojiano na suala hilo ambalo limekuwa moto kwenye mitandao ya kijamii.

Ommy alisema kwamba wanamitandao wanahisi kwamba sehemu za video ya wimbo Happy zinafanana na za video ya wimbo wa Bruno Mars uitwao “24k Magic”.

Mdundo wa wimbo huo nao, anadaiwa kuigiza mdundo wa wimbo wake Mr. Flavour uitwao “Big Baller”.

Akijibu tetesi hizo Diamond alisema kwamba baada ya kutoa wimbo Happy, aliona ukifananishwa na nyimbo za wasanii kama watano.

“Lakini nilifurahi kwamba vitu wanavyonilinganishia ni fikra za nje,” alijifariji Diamond akiendelea kusema kwamba watu wana haki ya kumkosoa na kamwe hana chuki nao kwa kufanya hivyo.

Katika maelezo yake, Diamond aliishia kusema kwamba yeye huwa haigizi bali hupata msukumo kutokana na fikra za wanamuziki wengine kisha anazungumza na mwelekezi naye anachangia maoni na wanatengeza kazi nzuri.

Msanii huyo alisema kwamba anafahamu fika kwamba sio kila mmoja anayemfuatilia ana fikra sawa kuhusu kazi zake.

Kuhusu minong’ono iliyosambaa mitandaoni kwamba Diamond au ukipenda Simba ameshindwa kumsaidia Mkubwa Fela mtu wake wa karibu ambaye amekuwa meneja wake tangu zamani.

Ommy alitanguliza kwamba Diamond ametumia zaidi ya shilingi milioni 100 kumsaidia mkubwa Fela huku Diamond naye akielezea kwamba alikuwa na Fela katika safari yake ya matibabu.

Alisema aligharamia matbabu ya Fela hata akapendekeza kwamba iwapo madaktari wangeruhusu angempeleka nchini India kwa matibabu zaidi na ikafanyika hivyo na aligharamia.

Diamond alizuru studio zilizoboreshwa kwa muonekano mpya za Wasafi Fm ambapo pia alikuwa mgeni kwenye kipindi hicho cha Exclusive.

Share This Article