CPAC ndio kamati fisadi zaidi, adai Gavana Kachapin

Martin Mwanje
1 Min Read
Simon Kachapin - Gavana wa West Pokot

Taarifa ya Martin Mwanje na Stephen Ayiengo 

Gavana wa kaunti ya West Pokot Simon Kachapin ameishutumu vikali Kamati ya Seneti ya Uhasibu wa Fedha za Umma za Kaunti, CPAC akiitaja kuwa fisadi zaidi.

Ameishutumu kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang kwa namna inavyoshughulikia masuala yanayohusu serikali za kaunti.

Kachapin sasa anamtaka Spika wa Seneti Amason Kingi kutilia maanani malalamishi ya Magavana kuhusu kamati hiyo akisema badala ya kuangazia masuala ya uwajibikaji, azma ya kamati hiyo huwa tu ni kuwataka Magavana kufika mbele yake.

Kulingana naye, hata Magavana wanapotii miito hiyo, CPAC huwa hulka ya kuwanyanyasa badala ya kutafuta suluhu kwa matatizo yanayokumba kaunti.

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo Baraza la Magavana limeitaka kamati hiyo kuondoa agizo la kukamatwa kwa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Agizo hilo lilitolewa na CPAC baada ya Sakaja kukosa kufika mbele yake mara nne.

Akiwahutubia wanahabari jana Jumanne, mwenyekiti wa CoG ambaye pia ni Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi pia alionya dhidi ya matumizi ya nguvu dhidi ya Magavana wanaokosa kufika mbele ya kamati hiyo.

Badala yake, ametoa wa malalamishi yaliyotolewa na Magavana kupigiwa darubini na uongozi wa bunge na kutafutiwa ufumbuzi kwa njia mwafaka.

 

Share This Article