Ruto aahidi kujenga soko la kisasa eneo la Gikomba

Rais Ruto anasema serikali yake inajenga jumla ya masoko 500 kote nchini katika hatua inayolenga kuwaepushia wafanyabiashara kero katika pirikapirika zao za kuchuma mali.

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ameahidi kujenga soko la kisasa katika eneo la Gikomba katika kaunti ya Nairobi.

Ruto amekanusha madai ya kuwatenga wafanyabiashara fulani katika mpango wa serikali wa kujenga soko la kisasa eneo hilo.

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi alipowahutubia wanawake wanachama wa Shirika la Maendeleo ya Wanawake nchini, kiongozi wa nchi amesema serikali yake imetenga shilingi milioni 800 zitakazotumika katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa soko hilo.

Shilingi zingine bilioni 5 zitatumiwa katika kujenga soko hilo lenye ghorofa saba katika awamu zijazo.

“Hakuna serikali imefikiria soko la Gikomba,” alisema Ruto wakati akilalamikia mazingira mabovu yanayowatesa wafanyabiashara katika soko hilo.

“Kukinyesha, wanavaa gambuti, kwa sababu pale ni matope, sewage inaenda kwao, wanunuzi wao hawakuji, shida kubwa. Mimi nimewaeleza hiyo Gikomba nitaibadilisha, iwe soko ya kisasa na watafanya biashara mahali pazuri.”

Aliongeza kuwa awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa soko litakalotumiwa na wafanyabiashara 5,000 kwa kima cha shilingi milioni 800.

“Nimeweka tena bilioni 3 zingine, halafu nitajenga sasa soko la shilingi bilioni 5 hapo hapo Gikomba,” aliongeza kiongozi wa nchi wakati akiashiria kuwa jumla ya masoko 500 yanajengwa na utawala wake kote nchini.

Wakati wa mkutano huo, Ruto alitoa wito kwa Wakenya kuepukana na viongozi wanaotaka kuleta migawanyiko miongoni mwao.

Amesema kuna haja ya Wakenya kujihadhari na viongozi wanaotaka kuwagawanya kwa misingi ya kisiasa au kikabila kwa manufaa ya nchi.

Hususan, alimkosoa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka akimtaka kuwaambia Wakenya alichowafanyia kwa kipindi cha karibu nusu karne alichokuwa madarakani.

 

 

 

Share This Article