Kenya hatimaye imelipa ada ya shilingi bilioni 3.9 zinazohitajika ili kuandaa kipute cha fainali za Kombe la Matifa ya Afrika, AFCON 2027.
Hatua hiyo inaodoa hofu kwamba Kenya ingefungiwa nje ya kuandaa kipute hicho kwani makataa ya kulipa ada hiyo ilikuwa jana Jumanne.
Nchi jirani za Tanzania na Uganda ambazo zilitaanda mashindano hayo pamoja na Kenya tayari zilikuwa zimelipa ada hiyo kwa Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF.
Tangazo la Kenya kulipa fedha hizo lilitolewa na Waziri wa Michezo Salim Mvurya kwenye taarifa jana Jumanne.
“Katika kutimiza ahadi zetu, serikali imelipa ada inayohitajika ya dola za Marekani milioni 30 kwa CAF, ikithibitisha tena uadilifu, utayari na dhamira isiyoyumba ya Kenya kuandaa mashindano hayo ya bara la Afrika kwa ufanisi,” alisema Mvurya kwenye taarifa.
Pia alisema serikali imeunda kamati ya maandalizi inayowaleta wadau kutoka asasi mbalimbali ili kuhakikisha maandalizi kabambe kuelekea mashindano hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji nchini Kenya (KBC) Agnes Kalekye ni miongoni mwa walioteuliwa kuhudumu kwenye kamati hiyo ya watu 38 itakayoshughulikia maandalizi ya AFCON mwakani.
Kamati hiyo itaongozwa na Katibu Mkuu wa zamani wa CECAFA Nicholas Musonye ambaye pia aliongoza kamati iliyosimamia fainali za CHAN mwaka uliopita.
Musonye atasaidiwa na Rais wa FKF Hussein Mohammed na pia inawajumuisha wachezaji waliostaafu wakiwemo Dan Shikanda na McDonald Mariga ambaye pia ni Naibu Rais wa FKF.
Kamati hiyo imejukumiwa na kusimamia maandalizi yote yakiwemo ya viwanja, mikahawa, na usalama kabla na wakati wa fainali hizo.
Kenya itaandaa fainali za AFCON 2027 kwa pamoja na Tanzania na Uganda kati ya Juni 19 na Julai 18.