Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula ametangaza kifo cha mbunge wa eneo la Ol Kalou, David Njuguna Kiaraho.
Kiaraho alifariki asubuhi ya leo Jumapili, tarehe 29 Machi 2026, alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Nairobi.
Njuguna amekuwa akihudumu kama Mbunge wa eneo la Ol Kalou tangu mwaka 2013, na alikuwa katika muhula wake wa tatu katika Bunge la Kitaifa.
Katika Bunge la 13, marehemu Kiaraho alikuwa anahudumu katika Kamati ya Uchukuzi na Miundombinu pamoja na Kamati ya Taratibu na Kanuni za Bunge.
Spika Wetangula tayari ameteua wabunge watakaounda Kamati ya maandalizi ya mazishi ili kushirikiana na familia ya marehemu mbunge huyo kuratibu shughuli za mazishi.
Mbunge wa Kinangop Kwenya Thuku ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo, akisaidiwa na mbunge wa Nyandarua Faith Gitau, pamoja na wabunge wengine saba.
Kifo cha kiongozi huyo kinajiri wiki chache tu baada ya kifo cha mwenzake wa Emurua Dikirr Johana Ng’eno aliyeaga dunia katika ajali ya ndege.