Rais William Ruto amesema Kenya inadhamini ushirikiano wake wa miaka 60 Umoja wa Mataifa, akidokeza kuwa umepandisha ngazi jiji la Nairobi na kulifanya kuwa kituo maarufu cha Umoja wa Mataifa sawia na New York, Geneva, na Vienna.
Rais Ruto aliyasema hayo leo Ijumaa aliposhiriki mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu watoto (UNICEF), Catherine Russell katika ikulu ya Nairobi.
Kwenye mkutano huo kiongozi wa taifa alielezea umuhimu wa shirika hilo katika kuleta mabadiliko kwenye sekta ya elimu kupitia mtaala wa masomo wa CBC, pamoja na kusaidia kwenye jitihada za kupunguza vifo vya kina-mama wanapojifungua.
“Tunadhamini ushirikiano dhabiti ambao tumekuza na Umoja wa Mataifa katika muda wa miaka 60 ambao umepandisha hadhi ya Jiji la Nairobi kuwa kitovu kikuu cha UN sawia na New York, Geneva, na Vienna,” alisema Rais Ruto.
Alisema walikubaliana kuhakikisha taifa hili lina mifumo bora ya afya na elimu, kutokana na ushirikiano unaowanufaisha raia wa Kenya.