EACC yarejesha shilingi milioni 13 katika kashfa ya ardhi ya makaburi

Martin Mwanje
2 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC, imepata kibali cha mahakama kurejesha shilingi milioni 13 kutoka kwa afisa wa zamani wa Baraza la Jiji la Nairobi lililovunjwa. 

Kibali hicho kinahusiana na kashfa ya ardhi ya makaburi ya kima cha shilingi milioni 283.

Fedha hizo zilirejeshwa kutoka kwa Mary Ng’ethe, ambaye alihudumu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Tathmini ya Kiufundi. Anadaiwa kupokea fedha hizo kama hongo ya kuwezesha ulaghai huo.

Kwenye uamuzi wake, Jaji Benjamin Musyoki wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi na Ulalifu wa Kiuchumi alibaini kuwa Ng’ethe alikuwa mhusika mkuu katika kashfa hiyo.

Mahakama ikisema alianzisha na kuongoza mchakato wa utoaji zabuni kwa njia ya ulaghai, na kwamba fedha alizopokea zilikuwa zawadi ya kuhusika kwake.

Mahakama pia ilisema fedha hizo ni za umma na lazima zirejeshwe.

Uchunguzi wa EACC ulibaini kuwa Baraza la Jiji la Nairobi lililpoteza kiasi kikubwa cha fedha za umma katika ununuzi wa ardhi kwa njia ya ulaghai. Ardhi hiyo ilikusudiwa kutumiwa kama makabauri  chini ya ilani ya zabuni nambari CCN/MOH/T/020/08/09 kwa thamani ya shilingi milioni 283.

EACC ikibaini kuwa ardhi hiyo haikufaa kwa matumizi ya makaburi na kwamba bei ya mkataba iliongezwa kwa kiwango cha juu zaidi.  Kati ya kiasi jumla cha fedha, milioni 110 zililipwa kwa mmiliki aliyesajiliwa, huku zilizosalia zikigawiwa miongoni mwa watu waliowezesha ulaghai huo.

EACC imeapa kurejesha mali yote ya umma iliyoibwa na kuwawajibisha wahusika.

Share This Article