Trump kufanya ziara ya siku mbili nchini China mwezi Mei

Martin Mwanje
1 Min Read
Marais Donald Trump wa Marekani na Xi Jinping wa China / Picha kwa hisani ya Reuters

Rais wa Marekani Donald Trump atafanya ziara ya siku mbili nchini China mwezi Mei mwaka huu. 

Kulingana na msemaji wa Ikulu ya Marekani Karoline Leavitt aliyewahutubia wanahabari jana Jumatano, Trump ataitembelea Beijing Mei 14 na 15.

Wakati wa ziara hiyo, atakutana na Rais wa China Xi Jinping na kufanya mazungumzo yatakayoangazia mada mbalimbali.

Ziara hiyo awali ilipangwa kufanywa kuanzi Machi 31 lakini upande wa Marekani ulitaka iahirishwe kutokana na operesheni za kijeshi nchini Iran.

Operesheni hizo zinafanywa na Marekani pamoja na Israel.

Mgogoro huo Mashariki ya Kati umesababisha usumbufu mkubwa wa usafirishaji bidhaa duniani hasa mafuta, hali ambayo imefanya bei ya bidhaa hiyo kuongezeka.

Alipoulizwa ikiwa mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati yatakuwa yametulia kufikia wakati wa ziara hiyo, msemaji huyo alisema utawala wa Trump umekadiria yamkini wiki nne hadi sita za mapigano.

Trump na Xi watakutana wakati ambapo nchi zao zimekuwa zikijiingiza katika migogoro ya biashara mara kwa mara.

Haijulikani ikiwa kukutana kwao kutasaidia kutuliza migogoro hiyo.

Share This Article