Rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete ameteuliwa kuwa Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Afrika, AU katika Upembe wa Afrika na Bahari ya Shamu.
Uteuzi huo umefanywa na Mwenyekiti wa Tume ya AU Mahmoud Ali Youssouf.
Kwenye wadhifa huo, Kikwete ataunga mkono jitihada za AU kuangazia masuala magumu ya kisiasa, amani na usalama katika kanda hiyo.
Kwenye taarifa, Youssouf anasema majukumu yake yatajumuisha kuendeleza diplomasia zuizi, kuwezesha mazungumzo jumuishi ya kisiasa, kuhamasisha ukuzaji wa imani miongoni mwa washikadau na kuimarisha mikakati ya ushirikiano wa kikanda unaodhamiria kukuza amani na uthabiti endelevu.
Pia atafanya kazi kwa karibu na washirika husika wa kikanda na wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na shirika la IGAD, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu na Umoja wa Mataifa miongoni mwa washikadau wengine katika juhudi za kuhamasisha amani, uthabiti na usalama.
Kikwete alihudumu kama Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2005-2015.