Usajili wa wapiga kura waanzishwa Chuo Kikuu cha Chuka

Haya yanajiri siku chache baada ya wanafunzi wa chuo hicho kukosa huduma katika afisi za IEBC walipokwenda kujisajili kama wapiga kura.

Marion Bosire
2 Min Read

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini, IEBC imepeleka huduma za usajili wa wapiga kura katika Chuo Kikuu cha Chuka katika kaunti ya Tharaka Nithi.

Haya yanajiri siku chache baada ya wanafunzi wa chuo hicho kulalamikia kutopata huduma katika afisi za IEBC walipokwenda kujisajili kama wapiga kura.

Meneja wa uchaguzi katika kaunti ya Tharaka Nithi Mohamed Raka aliomba radhi kuhusu hali hiyo akielezea kwamba siku hiyo maafisa wa IEBC walikuwa wamesafiri hadi Nairobi kwa ajili ya semina ya mafunzo.

Akizungumza afisini kwake, Raka alisema kuanzia siku ya Jumapili, wameweka mitambo miwili ya kusajili wapiga kura katika Chuo Kikuu cha Chuka, mashine ambazo zitasalia huko hadi wanafunzi wote wanaotaka kujisajili kama wapiga kura watakaposajiliwa.

Kulingana naye, mtambo mwingine mmoja wa kusajili wapiga kura umepelekwa katika bewa la Chogoria la chuo hicho ambapo wanatarajia kusajili wanafunzi zaidi kama wapiga kura.

Raka alisema kwamba wameweka mikakati ya kuhakikisha usajili endelevu wa wapiga kura katika sehemu mbalimbali za kaunti ya Tharaka Nithi wakiangazia taasisi za elimu ya juu pia.

Kando na Chuo Kikuu cha Chuka, IEBC inalenga pia Chuo Kikuu cha Tharaka katika eneo bunge la Tharaka.

Meneja huyo wa uchaguzi katika kaunti ya Tharaka Nithi ametoa wito kwa wanafunzi na wakazi wote wa kaunti hiyo kujisajili kama wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Share This Article