Tuju ajitokeza, asema alienda mafichoni kwa kuhofia maisha yake

Punde taarifa za kutoweka kwake zilipochipuka, kulikuwa na uvumi kwamba huenda Tuju alitekwa nyara kuhusiana na mzozo unaoghubika mali yake ya mamilioni ya pesa kwenye barabara ya Ngong. 

Martin Mwanje
2 Min Read
Mwanasiasa Raphael Tuju

Waziri wa zamani Raphael Tuju amejitokeza na kuwahutubia wanahabari, siku moja baada ya taarifa za kutoweka kwake kuibua dukuduku miongoni mwa Wakenya. 

Mbunge huyo wa zamani wa Rarieda alidaiwa kutekwa nyara juzi Jumamosi.

Punde zilipochipuka, kulikuwa na uvumi kwamba huenda Tuju alitekwa nyara kuhusiana na mzozo unaoghubika mali yake ya mamilioni ya pesa kwenye barabara ya Ngong.

Hata hivyo, akiwahutubia wanahabari leo Jumatatu mtaani Karen, Tuju amesema alienda mafichoni kwa kuhofia maisha yake.

“Nilikuwa naandamwa, kwa sababu ni rahisi kufahamu ikiwa unaandamwa. Unaendesha gari, unapunguza kasi, unapita gari lingine na wanajaribu pia kupita. Na baada ya tukio hilo, bila shaka, nilipiga ripoti kwa kituo cha polisi cha Karen,” alisema Tuju akiwa ameandamana na wanasiasa kadhaa na mawakili wake.

“Kilichonitia hofu zaidi ni kwamba gari lililoniandama halikuwa na nambari za usajili. Na baada ya kushuhudia wiki jana takriban landrova zaidi ya 20 za polisi zikija katika makazi yangu, na baadhi ya landrova hizo hazikuwa na nambari za usajili, nilihofu sana. Nilikuwa na msaidizi wangu lakini ni mimi nilikuwa naendesha gari, kufikia wakati nilipofika mzunguko wa Karen, walinikaribia zaidi. Hapo ndipo niliamua kupiga kona na kutoweka.”

Awali, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI wathibitisha kupokea taarifa za kutoweka kwa Tuju jana Jumapili na kuanza uchunguzi mara moja.

Maafisa hao wakilalama kuwa juhudi zao za kufika nyumbani kwa Tuju ili kufanya uchunguzi wao ziliambulia patupu.

Upinzani ulikuwa umezidisha miito ya vyombo vya usalama kufanya kila viwezalo hili kuhakikisha mwanasiasa huyo anapatikana.

 

Share This Article