Kenya imetoa changamoto kwa nchi zilizoendelea na wawekezaji duniani kote kusaidia katika ufadhili wa kilimo cha kisasa barani Afrika.
Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe anasema kushindwa kufanya hivyo kutakuwa na athari kubwa kwa mifumo ya chakula duniani.
Kagwe aliyasema hayo wakati wa Kongamano la 3 la Biashara la Mabadiliko ya Tabia Nchi Duniani kwa Afrika lililofanyika jijini Nairobi.
Waziri huyo akielezea umuhimu wa kubadilisha kiini cha mazungumzo kutoka kwenye hatari hadi dharura, na kuielezea Afrika siyo kama mwathiriwa wa mabadiliko ya tabia nchi, bali kama mstari wa mbele katika usalama wa chakula duniani.
Kulingana naye, mabadiliko ya tabia nchi tayari yanavuruga mifumo ya kawaida ya kilimo kote nchini Kenya, huku hali mbaya zaidi za hewa zikidhihirika nchini humo.
“Mabadiliko ya tabia nchi siyo kamwe hatari za siku zijazo — ni hatari za sasa. Ikiwa kilimo barani Afrika kitashindikana, mifumo ya chakula duniani itahisi athari za kushindikana huko,” alionya Kagwe.
Alificuhua kwamba hatua ya Kenya kutegemea mno kilimo cha mvua — kinachochangia asilimia 98 ya kilimo — inawafanya mamilioni ya Wakenya kukumbwa na hatari ya mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema madhara yamekuwa bayana kama ilivyodhihirishwa na misimu mitano ya kukosekana kwa mvua kati ya mwaka 2020 na 2023.
Aidha, aliashiria kuwa watu milioni 4.4 walikabiliwa na uhaba wa chakula na mifugo zaidi ya milioni 2.5 kufariki.