Serikali ina mpango wa kujenga kituo cha uokoaji katika kaunti ya Homa Bay ili kushughulikia dharura za Ziwa Viktoria na za kiusalama katika eneo hilo.
Rais William Ruto anasema serikali imetenga shilingi milioni 250 zitakazotumika kujenga na kuweka vifaa kwenye kituo hicho.
Akizungumza huko Homa Bay, Ruto aliashiria kwamba kituo hicho kitalenga wanaosafiri majini watakaopata ajali pamoja na wavuvi wa Ziwa Viktoria.
Alifichua mipango ya serikali ya kutumia Ziwa Viktoria kama raslimali muhimu akilitaja Ziwa hilo kuwa muhimu katika kubadilisha maisha ya Wakenya wengi wanaojihusisha na uvuvi na huduma za usafiri.
Ruto alisisitiza kwamba ni jukumu la serikali kulinda Ziwa Victoria na wanaojipatia riziki huko kwa kuwapa huduma stahiki kama vituo vya uokoaji.
Ahadi nyingine aliyotoa kiongozi wa nchi kwa watu wa Homa Bay ni ununuzi wa motaboti kwa gharama ya shilingi milioni 70 ili kutumika kushika doria Ziwani humo na kushughulikia visa vya dharura na ajali.
Rais alisema kwamba watu hufa maji kutokana na ukosefu wa vifaa stahiki vya kusaidia kuokoa maisha.
Kaunti ya Homa Bay itanufaika pia na miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu ya thamani ya shilingi bilioni 17 katika miji mbalimbali ya kaunti hiyo.