Millicent Omanga kugombea kiti cha mwakilishi wa wanawake Nairobi kwa DCP

Martin Mwanje
1 Min Read
Millicent Omanga akipokelewa DCP na Rigathi Gachagua

Sasa ni rasmi kwamba Seneta mteule wa zamani Millicent Omanga amekihama chama tawala cha UDA cha Rais William Ruto. 

Badala yake, amejiunga na chama cha DCP cha Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua.

Omanga alipokelewa katika ngome ya DCP na Rigathi katika hafla iliyoandaliwa hiyo jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.

“Hakuna kitu inawork Nairobi…Watu wetu wanauliwa kwa mafuriko na mimi nasema mkinipa huu uongozi wa kina mama, kuna vitu ambavyo haviwezi kuendelea hii Nairobi,” alisema Omanga ambaye awali aliwinda kiti cha mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Nairobi bila mafanikio.

Mwakilishi wa wanawake wa kaunti hiyo kwa sasa ni Esther Passaris ambaye ametangaza kwamba hatagombea wadhifa huo.

Passaris ametangaza kuwa anamezea mate kiti cha ubunge cha Makadara ambacho kwa sasa kinashikiliwa na George Aladwa.

Tangazo la Omanga lina maana kwamba huenda akakabiliana na Seneta mteule Karen Nyamu anayesemekana kumezea mate wadhifa huo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Share This Article