Washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati wakamatwa Kibra

Marion Bosire
2 Min Read

Maafisa wa Kitengo cha Kukabiliana na Dawa za Kulevya, ANU na wale wa Kitengo cha Kukabiliana na Ugaidi, ATPU wamefanikiwa kuharibu mitandao miwili ya ulanguzi wa dawa za kulevya katika eneo la Karanja, kaunti ndogo ya Kibra, kaunti ya Nairobi.

Walivamia nyumba moja ya makazi ya Ahmed Juma Wanjiru katika eneo hilo baada ya kupokea taarifa za kijasusi kwamba ilikuwa ikitumika kama kituo cha ulanguzi huo.

Msako uliotekelezwa katika nyumba hiyo ulipata vitu kadhaa vya kutiliwa shaka ikiwemo mimea iliyokaushwa inayoshukiwa kuwa midhadarati iliyokuwa imepakiwa kwenye mifuko.

Mifuko mitupu, mashine ya kupima uzani na pesa taslimu shilingi elfu 31,700, zinazoaminika kuwa mapato yaliyotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Mshukiwa huyo alitiwa mbaroni na nyumba yake ikakaguliwa vilivyo na maafisa hao wa usalama.

Operesheni nyingine katika eneo hilo ilihusisha nyumba nyingine ya makazi ambayo maafisa wa usalama walifahamishwa kwamba inatumika kwa biashara sawia.

Nyumba hiyo ya Sofia Burhan Marjan, nayo ilisakwa na maafisa wa usalama waliopata pakiti 7 za mimea iliyokaushwa inayoaminika kuwa dawa ya kulevya. Nyingine ilikuwa kwenye beseni huku misokoto kadhaa pia ikipatikana.

Katika nyumba ya pili maafisa walipata mashine za kupima uzani, makasi na vifaa vingine vinavyohusiana na maandalizi ya dawa za kulevya kabla ya kuziuza.

Kando na vitu hivyo, maafisa walipata risiti ya dhamana iliyo na jina la mshukiwa ishara kwamba aliwahi kuwa mkosaji akakamatwa na maafisa wa usalama akafikishwa mahakamani na kuachiliwa kwa dhamana.

Amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga akisubiri kufikishwa mahakamani.

Share This Article