Miguna Miguna amkosoa Bobi Wine

Anahisi kwamba bunge la Marekani sio mahali pazuri pa Bobi Wine kuanzia harakati zake.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanaharakati wa kisiasa nchini Kenya Miguna Miguna amemkosoa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine kuhusiana na harakati zake nchini Marekani.

Hii ni baada ya Wine kuchapisha picha inayomwonyesha akiwa nje ya majengo ya bunge nchini Marekani almaarufu Capitol Hill akisema kwamba hapo ndipo alianzia mashauriano yake ya kimataifa.

Kulingana na Miguna, eneo alilochagua Bobi Wine kuanzia harakati zake za kimataifa hapastahili.

“Mahali pabaya pa kuanzia na kupiga picha. Washington DC ni makao makuu ya ubeberu, mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu,” aliandika Miguna.

Mkenya huyo anayeishi na kufanya kazi nchini Canada aliendelea kusema kwamba hakuna mpenda Afrika halali au mpiganiaji uhuru ambaye hujivunia kile anachokitaja kuwa “ngome ya utumwa na unyama”.

Machi 14, 2026, Wine alichapisha video ambayo ilimwonyesha akielezea kwamba ameondoka Uganda kuelekea ughaibuni kwa mashauriano ya kile anachokitaja kuwa ukombozi wa Uganda ila hakutaja nchi aliyokwenda.

Msanii huyo wa muziki ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu aliwania Urais kwenye uchaguzi mkuu wa Januari nchini Uganda uliokumbwa na utata.

Alishindwa kwa mara ya pili kwenye kinyang’anyiro hicho na Rais Yoweri Museveni na baada ya uchaguzi, makazi yake yakazingirwa na maafisa wa polisi.

Bobi Wine aliweza kuondoka nyumbani kwake akaingia mafichoni tangu wakati huo hadi alipochapisha video ya kutangaza kuondoa kwake nchini Uganda.

Amekuwa akisisitiza kwamba aliibuka mshindi kwenye uchaguzi huo lakini ushindi huo ukabatilishwa ili kumpendelea Museveni ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 1986.

Inasubiriwa kuona hatua atakazopiga Wine katika mashauriano yake kimataifa.

Share This Article