Serikali ya Senegal imeelezea kusikitishwa kwake baada ya kamati ya rufaa ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuivua timu ya taifa ya nchi hiyo ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2025.
Kwenye uamuzi wake, CAF imetangaza Morocco kuwa mabingwa wa kombe hilo, hatua ambayo imeibua mdahalo mkali miongoni mwa wafuasi wa soka duniani kote.
“Uamuzi huo ambao haujawahi kutokea, wenye uzito usiokuwa wa kawaida, unakinzana moja kwa moja na kanuni za msingi zinazoongoza maadili ya michezo, kipaumbele miongoni mwa maadili hayo ikiwa ni usawa, uzalendo, na kuheshimu ukweli wa mchezo. Unatokana na ufasiri wenye dosari wa sheria, na kusababisha uamuzi ambao umepotoka kabisa kisheria na usiokuwa wa haki kabisa,” alisema Marie Rose Khady Fatou FAYE ambaye ni msemaji wa serikali ya nchi hiyo.
“Senegal haiwezi ikavumilia uamuzi wa kiutawala ambao unafuta dhamira, ustahiki, na ubobezi katika michezo. Senegal inakataa kabisa jaribio hili la uvuaji huu usiokuwa wa haki.”
Nchi hiyo sasa inatoa wito wa kufanywa kwa uchunguzi huru kuhusu ufisadi unaodaiwa kukita mizizi katika asasi ongozi za CAF.
“Isitoshe, Senegal itatumia njia zote mwafaka za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufika mbele ya mahakama zenye ustadi za kimataifa, kuhakikisha haki inadumu na ubora wa matokeo ya michezo unarejeshwa,” aliongeza FAYE kwenye taarifa.
Mechi ya Senegal na Morocco ilikumbwa na utata mkubwa baada ya wachezaji wa Senegal kususia kuendelea na mchezo wakipinga maamuzi ya mwamuzi, ikiwemo kutolewa kwa penalti dakika za mwisho wakati matokeo yakiwa 0-0.
Baada ya mchezo kusimama kwa takribani dakika 17 huku hali ya taharuki ikitawala uwanjani, wachezaji wa Senegal walirejea kucheza kufuatia kushawishiwa na mshambuliaji nyota Sadio Mane. Penati ya Morocco iliyopigwa na Brahim Diaz iliokolewa na kipa Edouard Mendy kabla ya Senegal kufunga bao la ushindi kupitia Pape Gueye katika muda wa nyongeza.
Hata hivyo, Morocco iliwasilisha rufaa kwa CAF, ambayo sasa imekubaliwa.
Katika uamuzi wa kushangaza uliotolewa siku 58 baada ya mechi, bodi ya rufaa ya CAF imesema Senegal imekiuka kanuni na hivyo “inachukuliwa kuwa imepoteza mchezo huo kwa kufungwa magoli 3-0,” na kuipa Morocco ushindi pamoja na ubingwa.
CAF pia imetoa adhabu mbalimbali, ikiwemo faini dhidi ya pande zote mbili, huku baadhi ya rufaa za Morocco zikikubaliwa na nyingine kukataliwa.
Uamuzi huo unaingia katika historia kama mojawapo ya maamuzi yenye utata kuwahi kufanywa katika soka ya Afrika.
Taarifa hii imechangiwa na BBC