Wavumbuzi nchini Uganda, wanajivunia kazi yao ya kuunda roboti ya kwanza kabisa ya kuelekeza watalii Barani Afrika.
Roboti hiyo inayoendeshwa na akili unde, imeundwa ili kubadilisha jinsi wageni wanafurahikia mandhari ya sekta ya utalii nchini Uganda.
Kazi hiyo iliyotekelezwa na wakfu wa ZunoBotics, ilizinduliwa rasmi Jumatatu katika hafla ambayo pia ilitumika kuzindua mashindano ya ulimbwende ya Miss Tourism Uganda mwaka 2026.
Roboti hiyo iliyopatiwa jina la “Okello”, inatarajiwa kuhudumu kama mwelekezi wa kidijitali aliye na uwezo wa kuwasiliana na watalii katika lugha mbali mbali akitoa habari muhimu kuhusu vivutio vya kitalii nchini humo.
Mwanzilishi wa wakfu wa ZunoBotics, Jonathan Ssemakula, alizungumza na wanahabari ambapo alisema kwamba mradi huo unalenga kuonyesha jinsi uvumbuzi wa kiteknolojia kama akili unde unaweza kutumika kuboresha utalii.
Ssemakula, ambaye ni mhandisi aliye na ujuzi kuhusu masuala ya roboti alielezea kwamba alishirikiana na wahandisi na wabunifu wengine katika kuafikia ufanisi huo.
Wahandisi na wabunifu hao hujumuika chini ya wakfu huo ambao ni kituo wazi cha masuala ya roboti na uwezeshaji kielektroniki ambacho hutumiwa na wanafunzi na wajuzi wanaotafuta suluhu kwa changamoto za Afrika.
Ssemakula alisema akili unde imekuwepo kwa muda na sasa inatumika katika sekta mbali mbali na walifika walipo kwa kujiuliza jinsi inaweza kusaidia sekta ya utalii.