Idadi ya vifo vilivyotokana na mafuriko nchini imeongezeka hadi watu 71 kutoka idadi ya awali ya watu 66, kwa mujibu wa Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS.
NPS imesema kwamba kaunti ya Nairobi ndiyo ina idadi kubwa ya maafa ambapo watu 36 wamefariki kufikia sasa kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa katika sehemu mbali mbali za nchi.
Eneo la Mashariki mwa nchi limenakili vifo 19, Bonde la Ufa vifo 8, Nyanza 4, Pwani 3 na eneo la kati mwa nchi kifo kimoja.
Mafuriko hayo yamesababisha pia familia zaidi ya 2,600 kupoteza makazi huku mali ya thamani isiyojulikana ikiharibiwa.
Katika taarifa, NPS ilielezea kwamba inashirikiana na asasi husika katika shughuli za kutafuta na kuokoa katika sehemu mbali mbali za nchi.
Huduma hiyo vile vile imeonya kwamba mvua inatarajiwa kuendelea kunyesha kwa kiwango kikubwa wakati huu ambapo msimu wa mvua ya masika inatarajiwa kuanza na kuendelea hadi mwezi Mei.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, KMD imetangaza kwamba mvua inatarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu masgariki na magharibi mwa Bonde la Ufa, eneo la Ziwa Viktoria, maeneo ya nyanda za chini kusini mashariki na Pwani.
Huku maeneo ya kaskazini mashariki na kaskazini magharibi yakitarajiwa kusalia kavu, mvua huenda ikashuhudiwa mara kwa mara na wakazi wanashauriwa kusalia macho.
Joto huko Pwani, kaskazini mashariki na kaskazini madharibi mwa nchi linatarajiwa kufikia nyuzi 30, na katika maeneo ya nyanda za juu joto huenda likapungua hadi nyuzi 10 usiku.
Umma unashauriwa kusalia macho, kufuata maelekezo rasmi na kuripoti matukio ya dharura kupitia nambari 999, 911, 112, 0800 722 203 au WhatsApp nambari 0709 570 000.