Michael B Jordan ndiye mshindi wa tuzo ya Mwigizaji Bora katika awamu ya 98 ya tuzo za Oscar, zilizoandaliwa usiku wa Machi 15, 2026 katika ukumbi wa Dolby ulioko Hollywood, Los Angeles nchini Marekani.
Hii ndiyo mara ya kwanza kabisa Jordan anashinda tuzo ya Oscar na aliwapiku washindani wenye nguvu kama Timothée Chalamet kwa filamu Marty Supreme, Ethan Hawke kwa Blue Moon na Leonardo DiCaprio kwa One Battle After Another.
Jordan alituzwa kutokana na jukumu lake kwenye filamu iitwayo “Sinners” ya Ryan Coogler ambapo anaigiza kama pacha wawili ambao ni Smoke na Stack.
Akiwa jukwaani kupokea tuzo yake, Jordan alisema, “Mungu ni mwema,” kisha akamgeukia mamake aliyekuwa amekaa naye katika ukumbi, na akasalimia wanafamilia wengine.
Msanii huyo alimmiminia sifa Ryan Coogler, ambaye amefanya naye kazi mara tano, akisema ana heshima kubwa kumwita mshirika na rafiki.
Alimshukuru kwa kumpa nafasi na mazingira yaliyomsaidia kuonekana.
Jordan wa umri wa miaka 39 sasa anaungana na orodha ya waigizaji weusi waliotukuka waliowahi kushinda tuzo ya mwigizaji bora kama Forest Whitaker kwa filamu ya The Last King of Scotland ya mwaka 2007, Denzel Washington kwa filamu ya Training Day ya mwaka 2002 na Sidney Poitier kwa filamu Lilies of the Field ya mwaka 1964.
Alitaja pia waliomtangulia kama Will Smith na Jamie Foxx, akiwashukuru wote waliokuwa katika ukumbi wa Dolby na kila mtu nyumbani kwa kuunga mkono kazi yake.
Jordan amekuwa na msimu mzuri wa tuzo, akipata uteuzi katika tuzo za BAFTA, Golden Globes na Critics’ Choice na kushinda kwenye Screen Actors Guild Awards tarehe 1 Machi.
Ushindi huo, muda mfupi kabla ya upigaji kura wa Oscars kufungwa, ulionekana na wengi kumpa Jordan msukumo muhimu katika hatua ya mwisho ya mashindano.