Mudavadi aelekea Moscow kwa mazungumzo ya ushirikiano

Ziara hiyo ya kikazi, inalenga kuimarisha uhusiano wa ushirikiano wa pande mbili kati ya Kenya na Shirikisho la Urusi.

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri aliye na mamlaka makuu na Waziri wa Masuala ya Nje, Musalia Mudavadi, ameondoka kuelekea Moscow, Urusi, kwa ziara ya siku mbili.

Ziara hiyo ya kikazi, inalenga kuimarisha uhusiano wa ushirikiano wa pande mbili kati ya Kenya na Shirikisho la Urusi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa afisi ya Waziri aliye na mamlaka makuu, ziara hiyo itazingatia kupanua ushirikiano katika sekta muhimu zikiwemo elimu, uhamiaji wa wafanyakazi, afya, miundombinu na nishati.

Serikali imesema safari hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi huku ikichunguza fursa mpya za biashara kati ya nchi hizo mbili.

Wakati wa ziara hiyo, Mudavadi anatarajiwa kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, pamoja na maafisa kutoka wizara zinazohusika na elimu na ajira.

Pia atatoa mhadhara wa hadhara katika Taasisi ya Moscow ya Mahusiano ya Kimataifa.

Kenya imetambua msaada wa Urusi katika sekta ya elimu kupitia programu za ufadhili wa masomo na katika kuimarisha uzalishaji wa kilimo kupitia msaada wa mbolea.

Mudavadi alibainisha kuwa kuna fursa kubwa ya kuongeza mauzo ya kahawa, chai na maua kutoka Kenya kwenda soko la Urusi, hasa wakati ambapo mazingira ya biashara ya kimataifa yanaendelea kubadilika.

Ajenda muhimu ya ziara hiyo itakuwa ustawi wa Wakenya wanaoishi, kusoma na kufanya kazi nchini Urusi. Mazungumzo hayo pia yataangazia wasiwasi kuhusu Wakenya ambao huenda walijiunga kwa hiari au bila hiari katika jeshi la Urusi wakati wa vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Mudavadi pia atasukuma hatua za kuwezesha urejeshwaji salama wa Wakenya walioathirika na kuimarisha ulinzi dhidi ya ajira za nje zinazotolewa kwa njia ya upotoshaji.

Maafisa wamesema ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi pana za serikali kuhakikisha usalama na heshima ya Wakenya wanaoishi nje ya nchi.

Share This Article