Dolly Parton atoa taarifa kuhusu hali yake kiafya

Dolly aliahirisha maonyesho yake ya Vegas kutokana na matatizo ya kiafya ambayo hayakufafanuliwa wazi.

Marion Bosire
2 Min Read

Dolly Parton amesema anaendelea vizuri kabisa baada ya changamoto za kiafya zilizomlazimisha kuahirisha tamasha zake za Las Vegas msimu uliopita wa vuli.

Mwanamuziki huyo wa umri wa miaka 80, alitoa taarifa alipoonekana kwa mara ya kwanza kwa kiwango kikubwa baada ya miezi kadhaa.

Nyota huyo wa muziki wa country alifichua kwamba anajitunza vizuri kuhusu matatizo yake ya afya alipokuwa jukwaani kufungua Dollywood — bustani yake ya burudani iliyoko Tennessee — kwa msimu mpya, kulingana na video ya kituo cha habari cha WVLT 8.

Dolly alieleza kwamba alichoka sana na kuishiwa nguvu baada ya kifo cha mume wake wa muda mrefu, Carl Dean. Wawili hao walikuwa wameoana kwa miaka 58 kabla ya kifo chake mwezi Machi mwaka 2025 akiwa na umri wa miaka 82.

Mwimbaji huyo anadumisha mtazamo chanya, akiongeza kwamba alijifikisha mahali ambapo alihitaji kujijenga tena kiroho, kihisia, na kimwili.

“Lakini sasa mambo yote ni mazuri. Hali hiyo haikunizuia kuendelea.” Alisema Dolly.

Dolly aliahirisha maonyesho yake ya Vegas kutokana na matatizo ya kiafya ambayo hayakufafanuliwa wazi, ingawa wiki chache kabla yake alifichua kuwa alikuwa na matatizo ya figo.

Alikosa pia kuhudhuria sherehe ya kuorodheshwa kwenye ‘Hall of Fame’ kwa shirika la kimataifa la maeneo ya maonyesho na burudani kwa ajili ya eneo lake la Dollywood mwezi Novemba 2025.

Dadake, Freida, pia alishtua mashabiki aliposema mwaka jana mitandaoni kwamba alikuwa amekesha usiku kucha akimwombea dadake Dolly.

Freida baadaye alifafanua kwamba hakutaka kukushtua yeyote aliposema kwamba alikuwa anamwombea Dolly, akisema alikuwa hajisikii vizuri kidogo, na aliomba kwa sababu anaamini sana nguvu ya maombi.

Inaonekana kwamba mapumziko aliyochukua Dolly yamezaa matunda — na sasa yuko tayari kurudi tena jukwaani.

Share This Article