Mvua kubwa inatarajiwa kushuhudiwa katika kaunti ya Nairobi na viunga vyake kati ya leo Ijumaa na Jumamosi.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imewatahadharisha raia kuwa waangalifu kutokana na uwezekano wa kuwepo kwa mafuriko hususan kwenye maeneo yaliyo tambarare.
Haya yanajiri takriban juma moja baada ya mvua kubwa kunyesha katika maeneo kadhaa nchini Machi 6 na 7.
Mvua hiyo ilikuwa chimbuko la mafuriko yaliyowaua watu 49 katika maeneo kadhaa nchini.
Watu kadhaa pia walijeruhiwa, maelfu ya familia kuachwa bila makazi na mali ya mamilioni ya pesa kuharibiwa.
Jijini Nairobi, watu 27 walithibitishwa kufariki kutokana na mafuriko hayo huku familia kadhaa zikiachwa bila makazi.
Utawala wa Gavana Johnson Sakaja umenyoshewa kidole cha lawama kwa kusheheni rundo la utepetevu kwa kukosa kujitayarishwa kwa majanga.
Pirikapirika za kukabiliana na athari za baada ya mafuriko bado zinaendelea katika maeneo kadhaa nchini.