Mipango ya maandilizi ya sherehe za mwaka huu za Madaraka, inaendelea vyema , huku ujenzi wa uwanja utakaoandaa sherehe hizo ukitarajiwa kukamilika kwa wakati.
Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt. Raymond Omollo leo Alhamisi alisema wanakandarasi watajizatiti kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo unakamilika, ili kuandaa sherehe hizo.
Aliyasema hayo alipokagua ujenzi wa uwanja wa Wajir, ambao utaandaa sherehe za 63 za Madaraka, akiwa ameandamana na Kamati ya kuandaa Sherehe za Kitaifa.
“Uwanja huu umesalia asilimia 10 ukamilike, na tunatarajia utakamilika kufikia wiki ya kwanza ya mwezi Mei tunapojiandaa kwa sherehe za Madaraka,’ alisema Omollo.
Kulingana na katibu huyo, hatua ya kuandaa sherehe za Madaraka katika kaunti ya Wajir, imeashiria kujitolea kwa serikali kuhakikisha ujumuishaji wa kitaifa.
Dkt. Omollo alisema kwa kuandaa sherehe hizo kwa mzunguko, kunawapa wakenya fursa ya kuwa na uwakilishi na pia kujumuishwa katika ufanisi wa maendeleo ya nchi.
Katibu huyo alikuwa ameandamana na Makatibu wa Wizara Principal Dkt. Patrick Mariru (Ulinzi) na Teresia Mbaika (Uchukuzi wa angani).