Serikali inalenga kuajiri walimu 16,000 zaidi kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Rais William Ruto amesema idadi hiyo itafanya jumla ya walimu walioajiriwa na utawala wake kufikia 116,000.
“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, tumeajiri walimu 100,000 na, kabla ya mwisho wa mwaka huu, tutaajiri walimu wengine 16,000, na kutimiza ahadi yetu ya kupunguza uhaba wa walimu 116,000,” alisema Rais Ruto wakati wa maadhimisho ya miaka 100 tangu kuasisiwa kwa shule ya upili ya Kapsabet, kaunti ya Nandi.
“Hii ndio idadi kubwa zaidi kuwahi kuajiriwa katika historia ya Kenya.”
Ruto alisema serikali yake inawekeza katika miundombinu ya elimu, akiashiria kuwa kwa kufanya kazi kwa karibu na wabunge, wamejenga madarasa zaidi ya 23,000 kote nchini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Isitoshe, ujenzi wa maabara za kisasa 1,600 umeanza kuhakikisha shule zinakuwa na vifaa vinavyotakikana, hasa katika nyanja muhimu za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.
Kulingana na kiongozi wa nchi, mgao wa sekta ya elimu umeongezeka kwa karibu asilimia 50 kutoka shilingi bilioni 500 mwaka 2022 hadi shilingi bilioni 702 katika mwaka wa sasa wa fedha.