Usimamizi endelevu wa maliasili umetambuliwa kama nguzo muhimu ya usalama wa taifa.
Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo amesema usimamizi wa kisasa wa usalama unahitaji maafisa kuangazia matumizi na ulinzi wa maliasili.
“Kwa kawaida, mamlaka yetu kama Idara ya Serikali yamehusishwa na kudumisha usalama. Hata hivyo, katika mazingira ya uongozi ya leo yanayobadilikabadilika, ni wazi kuwa usimamizi endelevu na ulinzi wa maliasili ni nguzo muhimu ya usalama wa taifa,” alisema Dkt. Omollo.
Akizungumza wakati wa warsha moja iliyoandaliwa mjini Eldoret na kuhudhuriwa maafisa waandamizi wa Wizara, Katibu huyo aliongeza kuwa ushindani wa rasilimali ikiwa ni pamoja na ardhi, maji, misitu na malisho umechangia mivutano na migogoro siku zilizopita.
Alitoa wito kwa maafisa hao kuangazia ukataji miti na kuingia katika misitu kinyume cha sheria kama sehemu ya majukumu yao ya kuhakikisha usalama wa nchi.
Alisema hali mbaya za hewa zimesababisha madhara nchini akitaja mafuriko ambayo yamethibitishwa kuua watu 49, kujeruhi wengi na kuharibu mali.
“Ukweli huu unatukumbusha kuwa kulinda maliasili si tu suala la uhifadhi, ni suala la kutunza mapato, kuzuia hali zinazoweza kusababisha migogoro, na utunzaji wa muda mrefu wa uthabiti wa nchi yetu,” aliongeza Dkt. Omollo.