Seneta wa kaunti ya Kilifi Stewart Madzayo ameomba ufafanuzi wa kina kuhusu madai ya unyanyasaji na vitisho vinavyodaiwa kufanywa na maafisa wa usalama dhidi ya waumini wa Kiislamu katika kaunti za Pwani.
Kulingana na Seneta huyo, wakazi hao wanahangaishwa wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hasa wanapohudhuria sala za Taraweeh nyakati za usiku.
Akiwasilisha ombi la kauli kwenye Kamati ya Seneti ya Usalama wa Taifa, Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni, Seneta Madzayo alisema suala hilo limezua taharuki miongoni mwa waumini na familia zao huku likiibua maswali mazito kuhusu uzingatiaji wa haki za kikatiba na taratibu za utekelezaji wa operesheni za kiusalama.
Alieleza kuwa madai ya kuzuiwa, kuhojiwa au kutishwa kwa waumini wanapokwenda au wanaporejea kutoka misikitini yamewaweka wengi katika hali ya hofu na siutofahamu hasa kwa kuzingatia kuwa ibada ya Taraweeh ni sehemu muhimu ya maadhimisho ya Ramadhani.
“Ni muhimu Kamati ieleze wazi mazingira ambayo matukio haya yameripotiwa, maeneo husika, hatua zilizochukuliwa dhidi ya maafisa wowote waliokiuka sheria na ni idara au ofisi zipi zilizoidhinisha operesheni hizo,” aliomba Seneta Madzayo.
Seneta huyo wa chama cha ODM alisisitiza kuwa Kamati inapaswa kubainisha iwapo kabla ya kutekelezwa kwa operesheni hizo, kulikuwa na mwongozo maalum uliotolewa kwa maafisa wa usalama kuhusu namna ya kuheshimu haki ya uhuru wa kuabudu kama ilivyoainishwa katika Katiba.
Aidha, aliitaka Kamati kufafanua iwapo kumekuwa na uchunguzi rasmi kuhusiana na madai hayo na kama waathirika walipewa fursa ya kuwasilisha malalamishi yao kupitia mifumo ya kisheria na kiutawala iliyopo.
Seneta Madzayo pia alitaka ibainishwe iwapo matukio hayo yanahusiana na ukosefu wa uratibu kati ya vyombo vya usalama na viongozi wa dini katika eneo la Pwani au kama kuna changamoto zingine za kiusalama zinazochangia hali hiyo.
Kadhalika, alitaka taarifa ya kina kuhusu hatua za muda mfupi na mrefu zilizowekwa kuhakikisha waumini wanaweza kuhudhuria ibada zao kwa amani bila hofu ya kunyanyaswa au kutishwa na mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya usalama na jamii.
Alikariri kuwa ni wajibu wa serikali kuhakikisha operesheni zote za kiusalama zinafanywa kwa kuzingatia Katiba, kuheshimu haki za binadamu na kuulinda uhuru wa kidini bila ubaguzi.