Rais Wiliam Ruto amesema kuwa hazina iliyobuniwa hivi karibuni ya miundombinu, itasaidia kupunguza bajeti, ushuru na madeni ya taifa hili.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa uuzaji wa hisa za kampuni ya usafirishaji mafuta ya Kenya Pipeline katika soko la hisa la Nairobi, kiongozi wa taifa alisema hazina hiyo itafadhili miradi mikubwa ya miundombinu hapa nchini.
Alisema uuzaji wa hisa za kampuni ya Kenya Pipeline umefanikisha kupatikana kwa shilingi bilioni 106 ambazo zitawekezwa ili kupata shilingi trilioni 1.2.
“Hivi ndivyo tutakavyobadilisha taifa hili,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa nchi aliwahakikishia wakenya kuwa mapato yanayotokana na uuzaji wa hisa za kampuni ya Kenya Pipeline, yatatumiwa kwa ustawi wa miundo msingi, na kwamba fedha hizo hazitaelekezwa kwa ulipaji madeni na mishahara.
Aidha alidokeza kuwa ubinafsishaji umesaidia kuimarisha dhamani ya mali ya umma ambayo tayari imekomaa.