Watu wasiopungua 15 wamefariki kwenye ajali katika barabara kuu ya Webuye-Kitale, jana Jumatatu usiku.
Ajali hiyo inadaiwa kusababishwa na dereva wa lori la masafa marefu ambaye alipoteza mwelekeo na kugonga magari kadhaa pamoja na wapita njia.
Akithibitisha ajali hiyo, kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Webuye Magharibi Rogers Bosire, alisema awali ajali ilitokea iliyohusisha pikipiki mbili na wakati umati ulipokusanyika kwenye eneo la ajali, dereva wa lori alipoteza mwelekeo na kugonga umati huo pamoja na magari yaliyokuwepo.
Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali ya kaunti ya Webuye kwa matibabu huku miili ya waliofariki ikipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo ikisubiri kutambuliwa na kufanyiwa uchunguzi.
Madereva wametakiwa kuwa waangalifu barabarani, hasa wakati huu wa msimu wa mvua ambapo barabara nyingi ni telezi.