Mwanamuziki tajika wa Uganda Jackie Chandiru amedai kwamba tasnia ya muziki katika taifa hilo la Afrika Mashariki imepoteza mwelekeo.
Mwanachama huyo wa kundi la muziki la Blu*3 alikuwa akizumgumza kwenye mahojiano ambapo alisema kwamba hali hiyo imechangiwa pakubwa na wasanii wa umri mdogo wanaotaka umaarufu wa haraka.
“Kutokana na hamu ya wasanii wa umri mdogo kujipatia umaarufu wa haraka, viungo spesheli vya muziki vimepotezwa,” alisema mwanamuziki huyo.
Alisisitiza kwamba kwa maoni yake, wanamuziki kwa sasa hawana mwelekeo na yeye ameamua kuwa na uwazi kuhusu suala hilo.
“Mtu anasema kitu, neno fulani linapata umaarufu na siku inayofuata linafanywa kuwa wimbo. Hakuna mwelekeo kabisa. Yeyote atakaye anaweza kuingia studio akaimba.” Aliendelea kusema Chandiru.
Nyota huyo wa muziki nchini Uganda sasa anahimiza wabunifu watafute kila mmoja nafasi yake maalum ma kuiangazia huku wakiimarisha ujuzi wao, badala ya kuingilia muziki kwa sababu tu wana ushawishi mkubwa mitandaoni.
“Iwapo wewe ni mwana-TikTok na ujuzi wako umejikita katika maigizo mafupi, kwama hapo. Imarisha ujuzi wako katika maigizo hayo. Usijaribu kuimba kwa sababu una wafuasi wengi,” alishauri.
Kulingana naye, hatua ya mtu kuingilia tasnia nyingine asiyoipendelea huenda ikafanikiwa au ikakosa kufanikiwa.
Haya yanajiri wakati ambapo kuna mdahalo kuhusu wasanii wa Uganda kujumuishwa kwenye matamasha ya kimataifa, mdahalo ambao umesababisha kuandaliwa kwa tamasha la Talanta Afrika Mashariki nchini humo.